Sunday, July 18, 2010

Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi ! AMEN!!


MWILI wa Profesa Jwan Mwaikusa aliyeuawa kwa kupigwa risasi nje ya nyumba yake huko Tegeta Salasala, jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, unaagwa leo katika Ukumbi wa Nkrumah, uliopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mtoto wa Profesa Mwaikusa, Msafiri aliliambia gazeti hili jana kuwa mara baada ya kutoka katika ukumbi huo saa 7:00 mchana, mwili huo utapelekwa nyumbani kwake, ambako ndugu na marafiki watatia heshima zao za mwisho kabla ya kuanza kwa shughuli ya maziko.

"Mpaka sasa bado hatujajua tutazika saa ngapi, ila mwili wa marehemu utafika hapa nyumba kesho (leo) saa 7:00 mchana na shughuli nyingine zitafuata. Inakuwa ngumu kueleza ratiba kamili kwa sababu pia yule ndugu yetu aliyeuawa siku moja na baba, naye inawezekana akasafirishwa kesho hiyo hiyo," alisema Msafiri

Ratiba iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ilionyesha kuwa mwili wa Profesa Mwaikusa, utatolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti saa 1:00 asubuhi ya leo.

Ratiba hiyo ya kumuaga Profesa Mwaikusa ambaye alikuwa Mhadhiri katika chuo hicho,ilionyesha kuwa baada ya mwili kufikishwa katika ukumbi wa Nkrumaha, kutakuwa na misa, itakayofuatiwa na shughuli za kutoa heshima za mwisho.

Hali kadhalika kutasoma historia ya marehemu.

"Watakaotoa heshima za mwisho kwa marehemu ni wahadhiri wa chuo hicho, wanasheria, wanafunzi, jumuiya mbalimbali, kitengo cha sheria cha chuo hicho, wananchi na wanafamilia," ilieleza ratiba hiyo.

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa mwili wa Profesa Mwaikusa, utaondolewa katika ukumbi wa Nkrumah saa 7 mchana na kupelekwa nyumbani kwake Tegeta Salasala, kwa maziko.

Profesa Mwaikusa aliuawa usiku wa kuamkia Jumatatu wiki hii, muda mfupi baada ya kurejea nyumbani kwake.

Mauaji hayo yalikuja baada ya watu wasiojulikana, kuvamia gari lake na kumtaka ashuke na baadaye kumfyatulia risasi mbili.

Kabla ya kumuua mwanazuoni huyo, watu hao walimuua mpwa wake, Gwamaka Mwakilasa kwa kumpiga risasi mbili mgongoni na baada ya matukio hayo mawili walikwenda nyumbani kwa jirani yake ambako walipora fedha, simu na vocha na baadaye kumuua mfanyabiashara, John Mtui ambaye anatarajiwa kuzikwa leo, huko Moshi mkoani Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment