
Babu akiwa na mtoto wake
MZEE mwenye umri wa miaka 90 ameushangaza ulimwengu baada ya kupata mtoto licha ya kuwa na umri huo mkubwa.
Babu huyo, Nanu Ram Jogi ambaye ni mkulima katika kijiji kimoja nchini humo amevunja rekodi yake ya kuzaa katika umri mkubwa ambayo aliishikilia kwa kipindi kirefu cha karne ya 21.
Mwanamume huyo ambaye ameoa mke wa nne katika ndoa zake, anasema hataacha kuzaa mpaka pale atakapotimiza umri wa miaka 100.
Jogi anasema kuwa bado hajapanga idadi kamili ya watoto anaowataka kutoka kwa wake zake hao wanne, lakini anapanga kuwa na watoto wa kiume angalau 12 na wasichana tisa huku akitaraji kuwa na wajukuu 20.
Paka aliyetoweka miezi mitatu arejea
BEDFRORDSHIRE, Uingereza
PAKA aliyewatoroka wenyeji wake miezi mitatu iliyopita amerejea nyumbani alipokuwa akiishi na kuwashangaza watu ambao walidhani kuwa pengine amefariki dunia.
Paka huyo anayejulikana kama alfie anayemilikiwa na Sylivia na Jon Callister alitopoka walipofika katika kituo cha biashara cha Toddington, Bedfordshire Uingereza, wakiwa safarini kurejea Hispania.
"Sikuamini nilipopigiwa simu na idara ya wanyama na kuambiwa kuwa amepatikana akiwa salama," alisema Bw Callister.
Padri aiba sadaka Sh102milioni
NEW HAVEN, Amerika
PADRI mmoja wa Kanisa Katoliki wiki hii aliwashangaza waumini wa kanisa hilo baada ya kuiba sadaka zenye thamani Sh102milioni.
Kiongozi huyo wa kanisa, Kevin J. Gray mwenye umri wa miaka 64 ni kati ya mapadri wanaoaminika, alichukua fedha hizo akiwalaghai waumini wake kwamba ana matatizo ya saratani.
Aliomba ahamishe kiasi cha fedha kwa ajili ya matibabu lakini kinyume na makubaliano ya kanisa, alizitumia kuwaburudisha wanaume pamoja na kuhudhuria matamasha ya watu waliokuwa wakicheza uchi na kununua nguo za bei mbaya.
Alikamatwa katika Hoteli ya Green and Arturo's, New York na kufunguliwa mashtaka yakiwemo ya kumlipia karo ya dola 1.3 milioni mwanamume aliyekutana naye katika bustani ya jiji la New York ili ahudhurie masomo kwenye Chuo cha Havard.
Bibi kizee amjeruhi vibaya mumewe kwa kikaango
MANILA, Ufilipino
MWANAMKE mmoja wa Ufilipino amefikishwa mahakamani baada ya kumjeruhi mumewe kwa kikaango kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Mwanamke huyo mzee wa miaka 50, Kimberly Denocheck alimpiga mumewe mwenye umri wa miaka 48 kwa kikaango hicho, majira ya saa 1: 25 asubuhi wakati alipokuwa akimwandalia kifungua kinywa. Kikaango hicho kilikuwa cha moto kwani ndiyo kwanza kilikuwa kimetoka jikoni.
Mwanamume huyo ambaye amepata majeraha makubwa kichwani, alifikwa na mkasa huo baada ya kuisahau simu yake ya mkononi jikoni hapo alipokuwa akiongea na mkewe na kisha ujumbe mfupi wa maandishi (sms) ukaingia na mkewe huyo kuisoma.
Polisi walisema kuwa mwanamke huyo bado anashikiliwa kituoni huku hali ya mwanamume ikiwa mbaya.
Zimeandaliwa na Herieth Makwetta
No comments:
Post a Comment